“If God doesn’t punish America, He’ll have to apologize to Sodom and Gomorrah.”
Mwinjilisti wa kimataifa, Billy Graham (95), amesema ikiwa Mungu hatashuka kuihukumu Marekani kutokana na kufanya uasi wa kila namna bila ya kuwa na hofu, basi itampasa aiombe radhi Sodoma na Gomora miji ambayo aliangamizwa kwa moto.
Rai hiyo aliitoa wiki chache zilizopita katika sherehe ya kuzaliwa, kwake ‘birthday’ iliyofanyika wiki iliyopita na kushuhudiwa na maelfu ya watu ambapo alisema kuwa wamarekani wamekuwa wakifanya dhambi kwa namna ya kutisha na sasa imefikia hatua mbaya, hawana tena hofu ya Mungu.
Mtumishi huyo ambaye amekuwa akihubiri watu zaidi ya bilioni mbili kwa wakati mmoja kwa kutumia vyombo vya habari alibainisha kwamba, Marekani ni taifa kubwa na watu wengi duniani wamekuwa wakiiga kila wanachofanya hivyo uovu wao haubakii kwao peke yao bali unaharibu sayari yote.
Alibainisha kwamba Mungu ni mwingi wa rehema, na kuwa ikiwa watamaanisha kutubu na kuziacha dhambi zao ni dhahiri kwamba atawasamehe na kuwarehemu, lakini wakishupaza shingo wataangamia kabisa.
Mwinjilisti huyo alisema ili kuikimbia ghadhabu ya Mungu, Wakristo wote nchini humo na mataifa jirani kama Kanada,wanapaswa kukusanyika kwenye majumba yao na marafiki, majirani na ndugu zao ili kushiriki ibada kwa pamoja kupitia Luninga zao aliyoiita “Living Room Crusade” kwa muda wa siku 40 kuanzia September 28 hadi November 6 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo.
Alisema amekuwa akihubiri kupitia Tovuti zake, na hilo ndilo litakalofanyika wakati wa kuomba msamaha, huku akibainisha kwamba, itapangwa siku maalum kwa ajili ya tukio hilo, ili kila mtu apate muda wa kushiriki; aweze kutubu, kumwomba Mungu awasamehe maovu yao ambayo ni zaidi ya Sodoma na Gomora.
Mwinjilisti huyo wa kimataifa ambaye amekuwa akimtumikia Mungu kwa miongo kadhaa sasa, alibainisha kuwa, katika kukusanyika pamoja kwenye majumba ya Wakristo, kila mmoja atapata wasaa wa kueleza uovu wake mbele za Mungu, huku akichanganua kuwa suala la utoaji wa mimba limekuwa kubwa.
Mbali na hilo, mtumishi huyo ambaye amekuwa akiwapa ushauri wa kiroho marais mbalimbali waliowahi kuitawala Marekani, akisisitiza juu ya hilo; alitolea mfano wa mji wa Ninawi ambao ulikithiri kwa dhambi, lakini Yona alipoingia na kuwaambia kutangaza kuwa utaangamia baada ya siku 40 walisikia na kutubu.
“Ninaamini msamaha walioupata wana wa Ninawi, unaweza kutokea na kwetu, Yona alipopita na kutangaza, waliitana na kutubu,” alisema Mwinjilisti Graham.
Miongoni mwa watumishi nchini humo waliounga mkono kauli hiyo ya Graham, ni pamoja na Mwenyekiti wa ‘American for Jesus’ Anne Gimenez ambaye siku hiyo ya kutubu atakusanya watu zaidi ya laki moja huko Philadelphia, alieleza kwamba, jambo kama hilo liliwahi kutokea kipindi cha nyuma Marekani na mataifa ya Ulaya baada ya kuibuka kwa mmomonyoko wa maadili na mambo ya kiroho.
“Nadhani wazo la Billy Graham ni sahihi, taifa hili linakuwa na watu wengi wasioamini, na jambo hilo linavyokuwa kwa kiasi hichi giza huingia, lakini kama tukiomba, basi nuru itaingia,” alisema.
Mwingine ni Mwandishi wa vitabu nchini humo, Rabbi Jonathan Cahn, kwa upande wake alieleza kwamba Mwinjilisti huyo wa kimataifa amekuwa Mchungaji kwa marais na watu maarufu kwa miaka mingi, na hilo analolisema sasa ni onyo linalopaswa kuangaliwa na kutendewa kazi.
“Haijalishi ni giza la namna gani lililopo, bado lipo tumaini na wokovu pia, lakini ni pale tutakapotubu na maombi ya watu wa Mungu, unajua akisema Marekani ina shida tunatakiwa kutubu,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Awakening America Alliance, Billy Wilson, alisema kwa upande wake atakusanya makanisa ya kipendekoste na Charismatic zaidi ya 300 na kwamba wamefurahia jambo hilo lililoletwa na Billy Graham.
Tangu mwaka 2002 mtoto wa Billy Graham, na mjukuu wake Will Graham, wamekuwa wakifanya uinjilisti katika mataifa kama 50 ya Ulaya, Afrika, Asia, Latini na Mashariki ya Kati na miongoni mwa makanisa yanayoshiriki ni zaidi ya 305,000 na kwa msingi huo watu wapatao milioni 10 wameweza kumgeukia Kristo.
Imeelezwa kwamba makusanyiko ya kusikiliza ujumbe wa Graham, yatayofanyika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwenye majumba ya kupata kahawa, na maduka yanafananishwa na mtoza ushuri nyakati za Biblia, kuwa baada ya kutubu dhambi aliamua kuita watu na kuwarudishia kile alichokuwa akitwaa kinyume na taratibu.
Wakati huo huo Askofu E. W. Jackson, mtaalamu wa mambo ya Maji na sheria kutoka chuo cha Harvard, nchini Marekani, amewataka Wakristo nchini humo, kutokichagua chama cha Democratic, katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika November, 2012 kwa kuwa kina imani potofu.
Mwandishi Paul Stanley, wa gazeti la Kikristo nchini humo anaripoti kuwa, hivi karibuni Askofu huyo alieleza kwamba chama cha Demokratic kinawaingiza utumwani baadhi ya waamerika.
“Waachieni watu wa Mungu waende,” alisema Jackson akiwaambia Wakristo kupitia mawasiliano ya simu ni wazi kuwa Democratic ni chama cha Mpinga Kristo katika nchi hii.Wameikataa Biblia na kile Wakristo wanachokiamini, na kuhamasisha kile watakacho wao kinyume na maadili ya familia. Hii ni mbaya kwakuwa wanalimomonyoa taifa na Mungu wetu,” alisema.
Askofu Jackson alinyooshea kidole habari za hivi karibuni kutoka kwa Waliberali waliomshambulia kwa maneno mwanamichezo wa Olympic, Gabrielle Douglas, mwenye umri wa miaka 16, aliyeshinda medali ya dhahabu huko London 2012 na kusoma Biblia, lakini wapenzi wa chama hicho wakamjia juu ya kuwa haikuwa sahihi.
Baada ya ushindi wa mwanariadha huyo alisoma maandiko kwenye Warumi 12:19, yasemayo: “Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa kisasi ni juu yangu mimi, mimi nitalipa, anena Bwana.” Mwanadada huyo mahiri aliazimia kumpa Mungu utukufu kwa ushindi wake,” alisema katika taarifa yake ya kimaandishi.
No comments:
Post a Comment